Waziri Mkuu afanya ukaguzi wa viwanja
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ukaguzi wa viwanja vitakavyotumiwa kufanya mazoezi na timu zitakazoshiriki michuano ya CHAN ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Agosti mwaka huu pamoja na michuano ya AFCON 2027 ikiwa ni ushirikiano wa nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda. Baada ya ukaguzi huo Waziri Mkuu, amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufanya tathmini ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwenye michuano hiyo. Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo jana Machi 29, 2025 baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata ambao ndiyo wakandarasi wa mradi huo.